Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNHCR awatembelea wakimbizi wa Nigeria kaskazini mwa Cameroon

Mkuu wa UNHCR awatembelea wakimbizi wa Nigeria kaskazini mwa Cameroon

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameanza ziara ya siku mbili Cameroon, ambayo inawapa hifadhi wakimbizi kutoka Nigeria na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Kwa mujibu wa mamlaka za jimbo la Kaskazini mwa Cameroon, zaidi ya wakimbizi 74,000 wa Nigeria wamevuka mpaka na kuingia kaskazini mwa Cameroon, wakiwemo 25,000 waliokimbia mapigano kati ya vikosi vya kikanda na wanamgambo kaskazini mashariki mwa Nigeria mnamo mwezi wa Februari pekee. Karin Gruijl ni kutoka UNICEF

"Kwa sababu ya hali tete kiusalama kwenye maeneo ya mpakani Kaskazini mwa Cameroon, UNHCR imekuwa ikiwahamishia wakimbizi hao kwenye kambi ya Minawao, iliyoko umbali wa kilomita 90 kutoka mji mkuu wa jimbo la Kaskazini, Maroua. Bwana Guterres atazuru Minawao kesho Jumatano kusikiliza ushuhuda wa wakimbizi moja kwa moja, na kujionea hali katika kambi hiyo ambayo ni makazi ya wakimbizi 33,000 wa Nigeria."

Kamishna Mkuu atakutana pia na baadhi ya raia wapatao 96,000 wa Cameroon ambao wamelazimika kuhama makwao kufuatia mashambulizi ya wanamgambo mara kwa mara nchini mwao, na kutoa msaada wa UNHCR ili kusaidia kukidhi mahitaji yao muhimu zaidi.