Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza ukeketaji Kenya ifikapo 2030 kunawezekana: wajumbe

Kutokomeza ukeketaji Kenya ifikapo 2030 kunawezekana: wajumbe

Mwelekeo wa kupunguza ukeketaji nchini Kenya unaleta matumaini ya kutokomeza mila hiyo inayoathiri wanawake na wasichana nchini humo.

Hii ni kwa mujibu wa Martha Tureti, mfanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali la World Vision linalohamasisha jamii nchini Kenya ili kuondoa vitendo vya ukeketaji.

Akizungumza na idhaa hii wakati wa  Mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake, CSW uliofanyika mjini New York, Bi Tureti amesema awali ilikuwa vigumu hata kuongea na jamii kuhusu mada hiyo lakini hivi sasa mtazamo wa jamii umebadilika, hasa tangu kupitishwa kwa sheria ya kupiga marufuku ukeketaji, mwaka 2011 na bunge la taifa la Kenya.

Bi Tureti amesema takwimu za 2007 zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana na wanawake nchini Kenya walikuwa wamekeketwa, akitumai kwamba idadi hiyo itazidi kupungua.

(sauti ya Martha)

Kwa upande wake Betty Naisenya, msichana mwenye asili ya kisamburu, ameshirikiana na Shirika la World Vision ili kuonyesha mfano wake wa kukataa ukeketaji na kuendelea na masomo.

Amesema maamuzi hayo yamemwendeleza kimaisha, na pia kubadilisha mtazamo wa wenzake na jamii yake kwa ujumla.

(Sauti ya Betty)