Dola Milioni 6.2 zahitajika kusaidia wakulima CAR

Dola Milioni 6.2 zahitajika kusaidia wakulima CAR

Wakulima huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wana mahitaji ya dharura ya mbegu na pembejeo kwa ajili ya msimu wa upanzi unaonza mwezi ujao, limesema shirika la chakula na kilimo duniani, FAO.

Katika taarifa yake, FAO imesema msaada huo wa dharura ni muhimu ili kuepusha kuzorota zaidi kwa usalama wa chakula na hali ya vipato vya wananchi kwenye nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo.

Mathalani watu Milioni Moja na Nusu hawana chakula hivi sasa na idadi hiyo inaweza kuongezeka, halikadhalika kiwango cha usaidizi iwapo msaada huo wa dharura hautapatikana.

Tayari FAO na wadau wake walishapata fedha kwa ajili ya kaya zaidi ya 86,000 zinazohitaji msaada wa dharura na sasa inahitaji nyongeza ya dola Bilioni Sita ili kusaidia shughuli za upanzi kwa msimu ujao kwenye kaya 63 600 zilizosalia.

Mwakilishi wa FAO nchini CAR Jean-Alexandre Scaglia amesema utekelezaji wa kampeni ya kilimo bila vikwazo vyovyote ni njia sahihi ya kupunguza mvutano wa kisiasa ambao ndio chanzo cha umaskini wa kupindukia.

Amesema kilimo kinasalia chanzo kikuu cha kipato kwa wananchi wengi wa CAR na kwamba kuwezesha upanzi, sambamba na harakati nyingine za kuimarisha uwezo wa wananchi kujipatia kipato ni jambo muhimu ili kuchangia jitihada za amani nchini humo.

FAO inasema kwa ujumla uzalishaji wa kilimo nchini Jamhuri ya AFrika ya Kati ni chini ya asilimia 60 ikilinganishwa na kipindi kabla ya kuanza kwa mzozo.