Baraza la Usalama laonywa kuwa Yemen yaelekea kusambaratika
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamekutana Jumapili mchana kuhusu hali Mashariki ya Kati, wakimulika taifa la Yemen ambalo mustakhbali wake umekumbwa na hali ya sintofahamu hivi karibuni.
Mshauri Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, Jamal Benomar, ameliambia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Qatar kuwa taiafa ya Yemen lipo kwenye mkondo wa kuelekea vita vya wenyewe kwa wenyewe. Amesema kwa wingi raia wa Yemen wanahisi kuwa hali inaendelea kuzorota kwa kasi.
“Wengi pia wanahofu kuwa mzozo umegeuka kuwa wa kidini, na kuongeza mgawanyo kati ya kaskazini na kusini. Kuna hofu pia kuwa kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Arabia litadakia fursa ya machafuko na kusababisha vurugu zaidi. Kufuatia mashambulizi ya bomu ya kujitoa mhanga, hisia zinazidi kuwa kali, na suluhu lisipopatikana hivi karibuni, taifa hilo litaingia katika machafuko zaidi na kusambaratika.”
Amesema baadhi ya watu wameanza kuhoji umuhimu wa kuwepo ofisi ya Umoja wa Mataifa na kuendeleza mazungumzo ya amani, lakini akaongeza kuwa hakuna njia mbadala ya kuboresha hali.
“Kuna watu wenye msimamo mkali kila upande ambao wangependa mazungumzo haya yafeli, na wamekuwa wakijaribu sana kuyavuruga. Tafadhali niruhusu nikariri kuwa, mazungumzo ya amani ndiyo njia pekee tuliyo nayo. Ni lazima nilinde hadhi ya mazungumzo hayo kama mpatanishi, na ni lazima niwe na nafasi ya kushauriana na pande zote, wakiwemo wale wanaovuruga kwa nguvu mpito wa kisiasa.”
Bwana Benomar amesema suluhu litapatikana tu iwapo pande zote husika zinajumuishwa katika mazungumzo, wakiwemo wapiganaji wa kundi la Houthi ambao wameripotiwa kuutwaa mji wa tatu mkubwa zaidi wa Taiz, na rais Abd-Rabbu Mansour Hadi ambaye alishakimbilia mji wa Aden.