Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ashukuru Italia kwa mchango wake kwenye UM

Ban ashukuru Italia kwa mchango wake kwenye UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa salamu za rambirambi kwa serikali ya Italia na wananchi kufuatia vifo na majeruhi vya raia wa nchi hiyo kwenye shambulio la Alhamisi huko Tunis Tunisia.

Ban ametoa rambirambi hizo mjini Turin wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Italia kuhusu ufadhili wa chuo cha watumishi wa umoja huo jijini humo.

“Nafahamu baadhi ya wakazi wa Torino wameuawa na pia kujeruhiwa, fikra zangu ziko nanyi. Tumekumbuka n ahata kuwa na dakika moja wakati wa kikao. Nafahamu kuwa mji wa Torino sasa uko kwenye maombolezo kwa siku mbili.”

Kuhusu makubaliano hayo, Ban ameshukuru serikali ya Italia kwa usaidizi wake kwenye chuo hicho cha mafunzo ya watumishi wa  Umoja wa Mataifa akisema kuwa mchango wa Euro 500,000 kila mwaka utazidi kukiimarisha na hivyo kuboresha huduma za chombo hicho duniani.

Halikadhalika ameshukuru mchango wa Italia kwenye operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa akitolea mfano walinda amani walioko Lebanon na kwingineko.