Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji kwa msingi wa ubaguzi wa rangi yakumbukwa na Baraza Kuu

Mauaji kwa msingi wa ubaguzi wa rangi yakumbukwa na Baraza Kuu

Mjini New York, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekutana leo kujadili kuhusu ubaguzi wa rangi, kesho tarehe 21 Machi ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi. Taarifa zaidi na Grace Kaneyia.

(Taarifa ya Grace)

Katika hotuba yake kwa niaba ya rais wa Baraza la Usalama, Sam Kutesa, Makamu Rais wa baraza hilo Mahmadamin Mahmadaminov amesema dunia inapaswa kukumbuka matukio ya uhalifu wa ubaguzi yaliyotokea zamani ili kuzuia vitendo kama hivyo visitokee tena.

Bwana Mahmadaminov amesema kwamba siku hiyo ya kimataifa huadhimishwa kila mwaka tangu 1966 kama kumbukizi ya mauaji ya watu 69 waliouawa wakiandamana dhidi ya sheria za ubaguzi mjini Sharpeville nchini Afrika ya Kusini, mwaka 1960.

“ Tunapaswa kuchukua mambo muhimu kutoka matukio hayo ya zamani, na kutumia ujuzi huu ili kupambana na vitendo vya ubaguzi wa rangi vinavyotokea siku hizi. Nalaani mashambulizi yaliyotokea hivi karibuni dhidi ya raia wa kawaida kwa misingi ya rangi, kabila au dini”

Akisisitiza kwamba kila mtu amezaliwa na haki sawa kama mwenzake, Makamu huyo wa Rais wa baraza kuu amesema suluhu ya ubaguzi wa rangi ni kuwezesha watu kuvumiliana na kufikia maridhiano ili kujenga jamii jumuishi.