Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utoaji chanjo uimarishwe kwenye nchi zilizodhibiti Ebola:WHO

Utoaji chanjo uimarishwe kwenye nchi zilizodhibiti Ebola:WHO

Shirika la afya duniani, WHO limetaka kuimarishwa kwa harakati za utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa kama vile surua, donda koo na mengineyo yanayoweza kuzuilika kwa chanjo kwenye nchi ambazo tayari zimedhibiti mlipuko wa Ebola.

Mkurugenzi wa chanjo WHO Dkt. Jean-Marie Okwo-Bele amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na kuripotiwa kwa visa vya surua kwenye nchi hizo.

(Sauti ya Dkt. Jean)

“Nchini Guinea kumeshukiwa wagonjwa 305 mwaka 2015 na watu wawili wamefariki dunia katika wilaya 10 zilizoripoti ugonjwa huo. Na hatimaye Sierra Leone visa 142 vimeripotiwa katika wilaya sita mwaka huu ambapo ni kifo kimoja.”

Amesema WHO tayari imetuma mwongozo wa utoaji chanjo kwa nchi zilizodhibiti Ebola huko Afrika Magharibi, mwongozo utakaozisaidia kuanzisha upya huduma za chanjo kwa njia salama kama vile kutumia sindano mara moja.

Tangu Ebola ilipuke mwezi Machi mwaka jana watu Elfu 24 wameambukizwa huku takribani Elfu 10 kati yao wakifariki dunia ambapo mlipuko huo ulisitisha huduma za chanjo za kawaida.

Surua hukadiriwa kusababisha vifo vya watu Milioni 2.6 kila mwaka iwapo hakuna kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo.