Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL huenda wametenda uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari- ripoti

ISIL huenda wametenda uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari- ripoti

Kundi linalotaka kuweka dola la uislamu wenye msimamo mkali, yaani ISIL, huenda limetenda aina tatu za uhalifu mkubwa zaidi wa kimataifa, mathalani uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ambayo imetolewa leo Alhamis na Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na timu ya wachunguzi waliotumwa kwenye eneo waliko ISIL na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu mwaka jana, imetokana na mahojiano na zaidi ya watu 100 ambao ama walishuhudia au walinusurika mashambulizi ya ISIL nchini Iraq kati ya Juni 2014 na Februari 2015.

Inaweka bayana msururu wa uhalifu uliotendwa na ISIL dhidi ya makundi kadhaa ya kikabila na kidini nchini Iraq, na ambao inasema huenda ukawa alifu wa mauaji ya kimbari.