Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna demokrasia Maldives bila haki: Mtaalamu

Hakuna demokrasia Maldives bila haki: Mtaalamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa majaji na wanasheria Gabriela Knaul ameonya kuhusu kudorora kwa kasi kubwa kwa uhuru wa mfumo wa haki nchini Maldives tangu afanye ziara nchini humo mwaka 2013.

Bi. Knaul amesema hayo wakati huu ambapo Rais wa zamani wa visiwa hivyo Mohammed Nasheed akiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 13 jela kwa makosa ya ugaidi kufuatia madai ya kuhusika na kutiwa ndani kwa hakimu wa mahakama ya uhalifu mwaka 2012.

Mtaalamu huyo amesema  ana wasiwasi mkubwa juu ya ukosefu wa misingi ya haki na uzingatiaji wa kanuni za mashtaka kwenye kesi dhidi ya rais huyo wa zamani.

Kwa mantiki hiyo amesihi serikali kuzingatia ripoti yake aliyowasilisha mwaka 2013 na itoe hakikisho kuwa mchakato wa kukata rufaa wa Bwana Nasheed utazingatia kanuni.

Halikadhalika ametoa wito kwa mamlaka za Maldives kuruhusu wananchi pamoja na waangalizi wa kimataifa walionyimwa haki ya kusikiliza kesi mara ya kwanza wahudhurie wakati wa rufaa.