Skip to main content

UM waitaka Pakistan isitishe adhabu ya kifo

UM waitaka Pakistan isitishe adhabu ya kifo

Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa visa na kasi ya kutekelezwa kwa adhabu ya kifo nchini Pakistan tangu mwezi Disemba 2014. Jingine la lililousikitisha umoja huo ni tangazo la serikali ya Pakistan hivi karibuni kuwa itaanza tena kutekeleza adhabu ya kifo kwa kesi zote, na wala si tu kwa kesi zinazohusiana na ugaidi.

Imeripotiwa kuwa miongoni mwa watu waliouawa ni wale waliokuwa watoto wakati walipofanya makosa. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kuwa kuna wafungwa 8,000 wanaosubiri adhabu ya kifo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Pakistan imesema inasikitishwa na baadhi ya kesi ambako watoto walinyongwa. Umoja wa Mataifa umetoa wito mauaji yote yakomeshwe kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia  kwa kosa alilolifanya akiwa angali chini ya umri wa miaka 18.

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa serikali ya Pakistan isitishe tena utekelezaji wa adhabu ya kifo, ikitaja kuwa, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amekariri mara kwa mara kuwa hukumu ya kifo haina nafasi katika karne ya 21.