Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lasikitishwa na kuvunjika kwa mazungumzo Sudan Kusini

Baraza la usalama lasikitishwa na kuvunjika kwa mazungumzo Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limesikiliza leo tathmini ya kusambaratika kwa mazungumzo ya amani baina ya pande zinazozozana Sudan Kusini, ambayo imewasilishwa na Haile Menkerios, Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Sudan na Sudan Kusini, na pia kuhusu Muungano wa Afrika, AU.

Kufuatia kuwasilishwa kwa tathmini hiyo, wanachama wa Baraza la Usalama wameelezea kusikitishwa na kuvunjika kwa mazungumzo hayo ya amani, na pia wasiwasi wao mkubwa kuhusu kuendelea mapigano na machafuko nchini Sudan Kusini.

Rais wa Baraza la Usalama François Delattre amewahutubia wanahabari mara tu baada ya mkutano wao, akisema wajumbe wa Baraza hilo wamekariri haja ya suluhu la kisiasa kwa mzozo huo, na wito wao kwa pande zote kujikita kwa hilo bila kuchelewa.

“Tumeelezea kuwa kwetu tayari kuunga mkono juhudi na michakato ya kufikia suluhu hilo. Tumekariri pia ahadi yetu ya kutekelezwa kikamilifu azimio namba 2206, na mwisho, tumekariri uungaji mkono wetu kwa UNMISS, ambayo hutekeleza majukumu yake katika mazingira magumu, na tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wa kikanda, hususan IGAD na AU.”