Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi Nigeria watoa hakikisho la uchaguzi huru na haki: Feltiman

Viongozi Nigeria watoa hakikisho la uchaguzi huru na haki: Feltiman

Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman amehitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Nigeria ambapo amekuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali wakiwemo wa kisiasa kutoka chama tawala na upinzani.

Halikadhalika amekutana na viongozi wa usalama, tume ya uchaguzi, wanadiplomasia na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa nchi za Afrika Magharibi Mohammed Ibn Chambas.

Bwana Feltman ametumia fursa hiyo kuwasilisha ujumbe wa Katibu Mkuu kuhusu mshikamano na nchi hiyo inapoelekea uchaguzi mkuu tarehe 28 mwezi huu.

Amesema anasubiri kwa hamu kuwasilisha salamu za hakikisho alilipatiwa na viongozi hao kuhusu uchaguzi huru na wa haki na unaozingatia ratiba.

Amewasisitiza wadau hao umuhimu wa kuendelea kushirikiana ili kuweka mazingira bora ya chaguzi huru na haki ili kila mwenye haki ya kupiga kura aweze kutekeleza haki hiyo ya msingi ya kikatiba ikiwemo waliopoteza makazi yao kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kutokana na ghasia.

Mkuu huyo wa masuala ya siasa amesema kwa upande wa Umoja wa Mataifa, Tume huru ya uchaguzi Nigeria imekuwa na maendeleo makubwa katika maandalizi ya uchaguzi ikiwemo usambazaji wa kadi za kudumu za mpiga kura licha ya muda mfupi na changamoto ya vifaa.

Kuhusu  mashambulizi yanayofanywa na Boko Haram, Bwana Feltman amerejelea msimamo wa Katibu Mkuu kuwa hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha ukatili unaofanywa na magaidi hao.