Gordon Brown aomba shule ziwe sehemu salama

Gordon Brown aomba shule ziwe sehemu salama

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Gordon Brown ametoa wito leo kwa mabadiliko ya msingi ili kuimarisha dhamira ya kimataifa ya kutetea haki za wanafunzi wa kike na wa kiume, akisema ni lazima mwaka 2015 uwe mwaka wa kusitisha ukiukaji wa haki za watoto.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Brown ambaye ni Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza amesema tunapaswa kufumbua macho juu ya mateso yanayokumba mamilioni ya watoto duniani kote.

Amesema shule zinazidi kulengwa wakati wa mizozo, na zaidi ya mashambulio 10,000 dhidi ya shule yametokea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, akitaja mifano ya Syria, Sudan Kusini, Pakistan na Nigeria.

"Nataka kuzingatia leo kwamba ni lazima kusitisha ukiukaji wa sheria ya kimataifa ambao unaathiri haki za mamilioni ya watoto. Sasa ni wakati wa kusitisha mwenendo unaozidi siku hizi wa kuteka watoto nyara kutoka shule ili kuwatumia kama silaha ya vita. Pia ni wakati wa kusisitiza kwamba, hata kwenye maeneo ya vita, kuna shule salama ambazo zinawezesha watoto kusoma kwa furaha na amani "

Bwana Gordon amependekeza kuunda mfumo wa fedha kwa ajili ya elimu wakati wa mizozo na pia akaiomba jamii ya kimataifa ijitahidi kuwapatia huduma za elimu wakimbizi wote kutoka Syria, hasa waliopo nchini Lebanon, kupitia masomo ya zamu.

Aidha ametangaza uzinduzi wa mfumo wa "shule salama" nchini Pakistan unaotumia teknolojia mpya inayoweza kuimarisha usalama na mawasilano ndani shule, utakaoanzishwa katika shule 1000 nchini humo.