Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua iliyofikiwa Haiti inafungua njia kufanyika uchaguzi: Honoré

Hatua iliyofikiwa Haiti inafungua njia kufanyika uchaguzi: Honoré

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Sandra Honoré amekaribisha hatua ya pande za kisiasa nchini humo za kuzingatia misingi ya mashauriano na kulegeza misimamo, mambo ambayo amesema yatafungua njia ya kufanyika kwa chaguzi zilizocheleweshwa kwa kipindi kirefu sasa.

Bi. Honoré ambaye ni Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti, MINUSTAH amesema hayo alipohutubia Baraza la usalama siku ya Jumanne jijini New York.

Amesisiza kuwa Haiti inaingia hatua ngumu ya uchaguzi na hivyo ametoa wito kwa serikali kupatia rasilimali za kutosha tume ya uchaguzi nchini humo ili iweze kutekeleza ipasavyo ratiba ya uchaguzi kama ilivyopangwa.

Sheria ya uchaguzi iliyopitishwa mwanzoni mwa mwezi huu wa Machi imetaja kuwa awamu ya kwanza ya chaguzi za bunge itafanyika tarehe Tisa mwezi Agosti mwaka huu.

Awamu ya pili ya uchaguzi huo pamoja na awamu ya kwanza ya uchaguzi wa Rais sambamba na uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika tarehe 25 mwezi Oktoba.