Demokrasia Myanmar, kuna dalili za kurudi nyuma: mtaalam wa UM
Mtalaam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Myanmar Yanghee Lee, ameziomba mamlaka za Myanmar kukubaliana na maswala yanayotatiza utaratibu wa demokrasia nchini humo.
Akitoa leo ripoti yake ya kwanza kuhusu Myanmar mbele ya Baraza la Haki za Binadamu, Bi Lee amesema kwamba vitendo kadhaa vya serikali vinaweza kuharibu mafanikio yaliyopatikana hadi sasa.
“ Kuna dalili za kurudi nyuma, ambazo zinatia wasiwasi, hasa jinsi nafasi kwenye jukwaa la demokrasia inavyopungua. Raia wengi, wanafunzi, ambao wanajaribu kueeleza kwamba hawakubali kufukuzwa kwao au wanapinga siasa ya serikali, hawawezi kusikiliza ipasavyo”
Amesema anasikitishwa sana baada ya waandamanaji na wanafunzi 127 kufungwa jela tarehe 10 Machi, pamoja na shinikizo linalowekwa juu ya waandishi wa habari.
Bi Lee amesesisitiza kwamba vyombo vya habari huru vina jukumu la msingi katika demokrasia.
Aidha ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya raia walioathirika na mapigano kwenye maeneo ya Kokang, magharibi mwa nchi, karibu ya mpaka na China.
Hatimaye Mtalaam huyo amezingatia umuhimu wa kuheshimu haki za watu kutoka makundi ya walio wachache, akitolea mfano waislamu wa jamii ya Rohingya kwenye wilaya ya Rakhine ambao bado wanakumbwa na unyanyapaa wa hali ya juu, akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kutafuta suluhu endelevu kwa jamii hiyo.