Nigeria yapiga hatua kuheshimu haki za makundi ya walio wachache: UM

Nigeria yapiga hatua kuheshimu haki za makundi ya walio wachache: UM

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu makundi ya walio wachache Bi Rita Izsak amesema kimsingi hakuna unyanyasaji wa makundi hayo nchini Nigeria.

Akilihutubia baraza la haki za binadamu mjini Geneva, mtaalmu huyo maalum amesema nchi hiyo imechukua hatua za kuhakikisha kila kundi katika kila ukanda nchini humo linajumuishwa ili kuepuka kupuuzwa kwa makundi madogo katika taifa hilo lenye idadi ya zaidi ya watu milioni 170.

Akitoa mfano Bi Izsak amesema Nigeria imeunda tume ya maendeleo mahususi kwa watu wa jimbo la Delta jambo linalosaidia ujumuishwaji wa ukanda huo. Hata hivyo ametoa angalizo.

"Haiwezekani kutokuwepo kabisa kwa matukio ya kutengwa kwa baadhi ya makundi. Ni muhimu kusisitiza kuwa vitendo kama hivyo haviungwi mkono na vyombo vya serikali. Kukomesha hili, serikali iendelee kutoa elimu ili kutokomeza chuki hizi."