Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yanatishia mustakhbali wa ukanda wa Sahel:UM

Mapigano yanatishia mustakhbali wa ukanda wa Sahel:UM

Mzozo unaoendelea kwenye ukanda wa Sahel barani Afrika unatishia harakati za kukwamua maisha ya maelfu ya watu ambao hali zao tayari ziko taabani kwenye eneo hilo.

Hayo ni kwa mujibu wa Robert Piper mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Sahel alipohojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.

Amesema mwaka mmoja uliopita pekee zaidi ya watu Milioni Moja wamepoteza makazi yao kutokana na mapigano kwenye nchi kadhaa za ukanda huo akitolea mfano Kaskazini mashariki mwa Nigeria na Kaskazini mwa Mali.

Halikadhalika ametaja matatizo ya kimuundo yanayokwamisha maendeleo ya nchi Tisa za ukanda huo wenye watu Milioni 145 hivyo amesema lazima hatua zichukuliwe.

(Sauti ya Piper)

"Urejee kwa wale ambao unajua wanatakiwa kuwajibika na hawa ni Serikali za maeneo ya Sahel, wao ndio pekee wenye uhalali, mamlaka na uwezo wa kutatua matatizo haya na pia urejee kwa washirika wa maendeleo kwa mfano benki ya dunia, UNDP, FAO na kadhalika, ili kuhakikisha wakati tunaendelea kuokoa maisha mwaka huu na mwaka kesho, tunapata muda wa kurekebisha miundo ya matatizo haya."

Kwa mujibu wa Piper katika ukanda wa Sahel watoto Milioni Moja nukta Mbili hufariki dunia kila mwaka ambapo chanzo cha vifo kwa nusu ya idadi hiyo ni utapiamlo.