Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA limehitimisha tathmini ya awali kuhusu hali ya kibinadamu katika visiwa vya Vanuatu baada ya kimbunga PAM kukumba eneo hilo.
Kwa mujibu wa OCHA, vifo 24 vimethibitishwa na watu 3,300 wametafuta hifadhi katika vituo 37 vya dharura. Tathmini hiyo iliyofanywa na ndege imeonyesha uharibifu mkubwa katika visiwa vya Vanuatu. Asilimia 80 ya wakazi bado hawana umeme, na mawasiliano ya redio na simu hayajarudishwa katika baadhi ya visiwa vilivyo mbali na mji mkuu Port Vila.
Wakati huo huo rais wa Vanuatu ametoa wito kwa usaidizi wa kimatiafa kutokana na uharibifu mkubwa ambao haujawahi kutokea kwenye nchi yake.
Aidha timu ya dharura ya OCHA imewasili leo nchini Vanuatu ili kuratibu misaada itakayotumwa katika siku zijazo. Tayari vyakula kadhaa vikiwemo mchele, maji, kahawa, sukari na biskuti vimesambazwa katika vituo vya dharura.