Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Michezo inasaidia kuonyesha uwezo wa wanawake- UN Women

Michezo inasaidia kuonyesha uwezo wa wanawake- UN Women

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka, amesema kuwa michezo ina umuhimu mkubwa kwa wanawake na wasichana, kwani mara nyingi inasaidia kudhihirisha uwezo wao.

Bi Mlambo-Ngcuka ameyasema hayo wakati wa mkutano ulioandaliwa na shirika la UN Women likishirikiana na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, wakati wa vikao vya 59 vya Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake. Mkuu huyo wa UN Women amesema jukwaa la Beijing lilitambua pia umuhimu wa michezo na elimu ya mazoezi ya mwili katika kuweka bayana nyota ya wanawake na wasichana.

“Umuhimu wa michezo kwa wasichana pia ni kudhihirisha ubora wa ustadi wao, na kusaidia kuwainua kutoka katika hali ambako wanahaha kupambana na hali ngumu, lakini vipaji vyao vinanawiri, na kwa njia hiyo, wanaweza kuibuka washindi katika hali ngumu. Na kupitia kushiriki michezo na kuishi kwa maadili yake, wanawake na wasichana wanaweza kukuza stadi za uongozi, kushinda ubaguzi, kuboresha afya yao na kuwezeshwa”.

Hata hivyo, amesema kuwa licha ya ufanisi wote huo wa wanawake, bado wengi wanakabiliana na itikadi za kijinsia, sio tu katika michezo lakini kwa kila sekta.

“Itikadi hizi, sio tu katika michezo, lakini katika sekta zote, hushusha hadhi ya wanawake. Tunaahidi kuwa mshirika thabiti- tayari tunashirikiana na IOC- na kupitia ubia huu, tunaona uwezekano wetu pamoja kuuinua ufanisi wanawake na wasichana.”

Amesema miaka 20 tangu jukwaa la Beijing, nchi zote zilizotathminiwa zimeonyesha kuboresha kwa sheria zinazokabiliana na ubaguzi dhidi ya wanawake, lakini utekelezaji bado ni hafifu, na mila na itikadi zinazoshusha hadhi ya wanawake bado ni thabiti.