Ban atoa mafunzo kutoka Japan

15 Machi 2015

Katika kongamano la tatu la Umoja wa Mataifa kuhusu kupunguza hatari za majanga linaloendelea mjini Sendai, Japan, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema hatuwezi kuzuia majanga kwani ni kuamua kwa mungu lakini tunaweza kupunguza hatari zao kwa kujitayarisha vizuri zaidi. Ameongeza kwamba bora kuwekeza pesa katika mifumo ya tahadhari kuliko kugharimu ukarabati baada ya uharibifu.

Akizungumza kwenye chuo kikuu cha Tohoku ambapo wanafunzi watatu walipoteza maisha wakati wa tetemeko kubwa la ardhi lililokumba maeneo ya Japan mashariki mwaka 2011, Katibu mkuu amesema Japan imejitahidi katika kuimarisha jinsi ya kuzuia hatari za majanga.

Amewapongeza wajapan kwa jitihada zao katika kukarabati mji wa Sendai na kubaki na matumaini licha ya matatizo waliyoyapitia.

Aidha ameshukuru serikali na raia wa Japan kwa msaada wao wanaoendelea kutoa kwa ajili ya kusaidi watu wanaoathirika na majanga duniani kote, huku Japan ikiwa imetangaza kuchangia dola bilioni 4 kwenye mfumo wa kupunguza hatari za majanga.

Halikadhalika Bwana Ban ametembelea vituo vya jamii huko Sendai na kiwanda cha kusafisha maji machafu kilichojengwa upya na kwa njia imara baada ya kuharibika wakati wa tsunami.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter