Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto nchini Syria wanashuhudia wafungwa wakinyongwa hadharani:UM

Watoto nchini Syria wanashuhudia wafungwa wakinyongwa hadharani:UM

Tabia ya watoto na vijana nchini Syria kukutanika pamoja na kuangalia video za watu wakinyongwa ni moja ya mambo ambayo yanatia hofu shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF) wakati mgogoro huo ukiendelea na kuingia mwaka wa tano.

Hayo yamesemwa na mfanyakazi wa UNICEF Hanaa Singer ambaye mwaka jana mzima amekuwa akiratibu misaada ya kibinadamu katika baadhi ya maeneo hatari zaidi nchini Syria ikiwemo mji wa Raqqah kaskazini mwa nchi hiyo ambayo vitendo vya unyongaji vinaonyeshwa hadharani.

Bi Singer amesema watu milioni 4.2 bado hawawezi kufikiwa katika maeneo yenye vita.

“ Kuna watoto milioni 5.6 walioathirika na mzozo, wengi wao wakiwa wamelazimika kuhama makwao. Wengi zaidi hawawezi kufikiwa na UNICEF, idadi ikiwa inaweza kufika milioni 2 au 3. Shule moja kati ya tano imebomolewa kabisa. Kila sehemu ya maisha ya watoto wa Syria imeathirika kwa njia moja au nyingine.”

Kwa ujumla, UNICEF imetangaza kuwa ni watoto milioni 14 ambao wameathirika na mzozo huo nchini Syria na nchi zingine.