Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nini kifanyike kumaliza vita na mateso Syria?:UM

Nini kifanyike kumaliza vita na mateso Syria?:UM

Viongozi wanane wa ngazi ya juu kwenye Umoja wa Mataifa wanasema mgogoro wa Syria ambao unaingia mwaka wa tano sasa unaendelea kukatili maisha ya watu na kuleta hasara kubwa, ukiwa ni mgogoro ambao jumuiya ya kimataifa imeshindwa kuusitisha. Taarifa kamili na John Kibego..

(TAARIFA YA JOHN KIBEGO)

Viongozi hao ambao ni Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani(WFP), Kamisha Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR), Mkuu wa Shirika la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura(OCHA), mwakilishi maalumu wa ukatili wa kimapenzi kwenye maeneo ya vita, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani(WHO), Kamisha Mkuu wa Shirika la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina(UNRWA),Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto(UNICEF) na mwakilishi maalumu wa watoto kwenye maeneo ya vita vya silaha , wamesema zaidi ya watu 200,000 wameshapoteza maisha Syria, huku watoto na vijana wakizungukwa na vurugu, kukata tamaa na kunyimwa haki.

Viongozi hao wameelezea hofu , uchungu na ghadhabu wakati wakishuhudia janga hili linavyoendelea. Wamesema wamejidhatiti kuendelea kufanya kila wawezalo kuwasaidia mamilioni ya watu waliojikuta wakatikati ya vita hivi, wakikosa suluhisho na pakukimbilia.

Wamewataka viongozi wa dunia kuweka kando tofauti zao na kutumia ushawishi kuleta mabadiliko nchini Syria, kuzishinikiza pande husika kukomesha mashambulizi dhidi ya raia na kuwanusuru zaidi ya 212,000 waliojikuta wamekwama bila chakula wala huduma zingine muhimu kwa miezi kadhaa sasa.