Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya wanawake uongozini Afrika yamulikwa New York

Hatma ya wanawake uongozini Afrika yamulikwa New York

Ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 imesisitiza umuhimu wa kuwezesha vijana ili kuleta maendeleo kupitia huduma za afya, elimu, teknolojia, na ajira. Hata hivyo, kuwapa wasichana fursa sawa katika mkakati huo bado ni changamoto.

Ni mada ambayo imeangaziwa leo kwenye mkutano maalum kuhusu uongozi wa wasichana na wanawake katika ajenda ya Afrika ya 2063, uliofanyika leo mjini New York wakati wa mkutano wa 59 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake, CSW.

Maged Abdelaziz, Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika, amesema bado wasichana wa Kiafrika wanakumbwa na changamoto nyingi zaidi, kutokana na jinsia na umri wao.

(Sauti ya Maged Abdelaziz)

"Kutokana na vikwazo vya kijamii, kiuchumi, kimazingira, kijiografia na kimila, wasichana wa kiafrika wanakumbwa na hali ya juu ya ukosefu wa ajira au ajira duni, pamoja na ukosefu wa huduma za elimu bora, mtaji, na huduma za afya ikiwemo afya ya uzazi"

Licha ya hayo, Bwana Abdelaziz ameeleza kwamba wanawake wamejitahidi kupigania haki zao, na kufanikiwa kuchukua uongozi katika sekta za uchumi, siasa, au ustawi wa jamii.

Bi Naisula Lesuuda, seneta na Naibu Mwenyekiti wa Shirika la Wanawake wabunge wa Kenya, amefafanua mafanikio yaliyopatikana Kenya katika uongozi wa kisiasa.

(Sauti ya Naisula Lesuuda)

"Katiba imeweka masharti kwamba kila jinsia inapaswa kuwakilishwa katika kila nafasi za kuchaguliwa au za kuteuliwa kwa angalau theluthi moja. Kwa hiyo Baraza la Mawaziri lina wanawake asilimia 33.3, na si tu wanawake, bali wameshika nafasi muhimu. Pia kwenye Bunge, leo wanawake ni asilimia 25 ya wabunge, kutoka kwa asimilia 9.9 mwaka 2007."