Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wako katika mazingira magumu Zaidi kwa sababu ya mlolongo wa migogoro:Zerrougui

Watoto wako katika mazingira magumu Zaidi kwa sababu ya mlolongo wa migogoro:Zerrougui

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya watoto na vita vya silaha Bi. Leila Zerrougui amesema mwaka 2014 umekuwa na migogoro mingi na imewaweka watoto katika mazingira magumu zaidi ya athari za vita.Bi. Zerrougui  ameyasema hayo wakati akiwasilisha ripoti yake ya mwaka  kwenye baraza la haki za binadamu mjini Geneva leo , ripoti ambayo imeunganisha matukio ya tangu Disemba 2013 hadi disemba 2014.

Ameongeza kuwa katika nchi sita ambazo zimeathirika vibaya saana na vita za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Iraq, Nigeria, Palestina, Sudan kusini na Syria watoto wamekuwa wahanga wa ukiukaji mbaya zaidi wa haki zao.

Kwa mujibu wa Bi Zerrougui mgawanyiko wa kikabila uliochochewa na mvutano wa madaraka pia umechangia pakubwa makundi yenye itikadi kali yanayotumia ghasia za kupindukia zinazowalenga watoto na watu wazima bila kujali wala kutofautisha wapiganaji na raia .

Amesema dunia imeshuhudia ukiukwaji mkubwa na mauaji yanayofanywa na kundi la ISIL au boko Haramu, ikiwemo mauaji, kuwaingiza watoto jeshini, ukataji viungo, unyanyasaji wa kijinsia na utumwa wa ngono , matumizi ya wasichana wadogo kama kafara kwa kujitoa muhanga na pia utekaji wa mamia ya watoto.

Amesema kuna maeneo manne ambayo kazi za baraza la haki za binadamu zinaweza kuboreshwa katika kuwalinda watoto, ikiwemo kukomesha ukwepaji sheria, kutafuta njia mbadala ya jela kwa watoto, kuwepo kwa rasilimali za kutosha kuwarejesha watoto waliokuwa jeshini katika maisha ya kawaida na kulinda shule na hospitali kutokana na mashambulio