Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu awafuata raia wa Eritrea nchini Ubelgiji

Mtaalamu awafuata raia wa Eritrea nchini Ubelgiji

Mtaalamu maalum wa haki za binadamu nchini Eritrea Sheila B. Keetharuth, ameanza ziara rasmi ya siku tatu nchini Ubelgiji kuanzia leo kwa lengo la kukusanya taarifa sahihi kuhusu hali ya raia wa Eritrea wanaoishi nchini humo kama wakimbizi au wahamiaji.

Taarifa ya Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imemkariri Bi. Keetaruthu akisema amechukua hatua hiyo baada ya kushindwa kuwafikia nchini Eritrea na amekuwa akiomba kibali cha serikali tangu mwezi Novemba 2012 bila mafanikio yoyote.

Kutokana na hali hiyo ameshatembelea Djibouti, Ethiopia, Ujerumani, Italia, Malta na Tunisia ili kuweza kuzungumza na raia hao wa Eritrea wanaoishi ughaibuni.

Akiwa ziarani humo mtaalamu huyo atawahoji wakimbizi na wahamiaji wa Eritrea ili kubaini uhalisia wa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Eritrea kwa mujibu wa ripoti alizopokea kutoka vyanzo mbali mbali.

Bi. Keetharuth ameshukuru Ubelgiji kwa kukubali kumpatia ruhusa ya kwenda nchini humo na kutekeleza jukumu lake na matokeo ya uchunguzi huo atayawasilisha kwenye ripoti yake ya tatu mbele ya baraza la haki za binadamu mwezi Juni mwaka huu.