Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio jingine Mali: UM walaani

Shambulio jingine Mali: UM walaani

Wanachama wa Bara za la Usalama wamelaani vikali shambulio jingine la kigaidi lililotokea leo nchini Mali, kwenye maeneo ya Kidal dhidi ya kambi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA.

Watoto wawili na mlinda amani mmoja kutoka Chad wamefariki dunia kwenye shambulio hilo, na wengine kujeruhiwa.

Wanachama wa baraza la Usalama wamepeleka salamu zao za rambirambi kwa familia za wahanga wa uhalifu huo, pamoja na serikali na raia wa Mali na Chad. Wametambua mchango mkubwa wa Chad katika MINUSMA.

Aidha wanachama wa Baraza hilo wameeleza kwamba uhalifu dhidi ya walinda amani unaweza kuwa uhalifu wa kivita kulingana na sheria ya kimataifa.

Halikadhalika wameziomba pande zote wajizuie na vitendo vinavyoweza kuathiri amani, na hivyo kukariri utayari wao wakuweka vizuizi dhidi ya wale ambao watavunja makubaliano ya kusitisha mapigano.