Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake bado wanakumbwa na madhila kwenye amani na vita:Ban

Wanawake bado wanakumbwa na madhila kwenye amani na vita:Ban

Leo ni siku ya wanawake duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema madhila yanayokumba wanawake na wasichana na watoto wa kike bado yanatikisa maeneo mbali mbali duniani.

Katika ujumbe wake wa siku hii ametolea mfano maeneo ambayo watoto wadogo wa kike wenye umri wa miaka saba wanatumiwa kama silaha ya vita na makundi yenye msimamo mkali ikiwa ni miongo miwili baada ya mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing ukilenga pamoja na mambo mengine kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Kwa mantiki hiyo ametaka dunia kuungana dhidi ya makundi hayo yaliyoko Nigeria, Somalia, Syria na Iraq ambayo yamegeuza miili ya wanawake kuwa uwanja wa vita kwa lengo la kukidhi matakwa yao.

Ban amesema kundi hilo pia linakumbwa na madhila linaposaka elimu na huduma ya msingi na hata wale wanaotaka kujitolea kuwapatia huduma kama vile madaktari na wauguzi.

Katibu Mkuu amesema hata kwenye baadhi ya maeneo yenye amani, wanawake na wasichana bado wanakumbwa na taabu ya kukwamishwa harakati zao za kujiendeleza.

Amesema bila kubadili mwelekeo itakuwa ndoto kufanikisha malengo ya maendeleo iwapo asilimia 50 ya wakazi wa dunia ambao ni wanawake wanaenguliwa.

Ujumbe wa mwaka huu ni Wezesha mwanamke, wezesha ubinadamu, pata picha ambapo jijini New York, shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya wanawake limeandaa maandamano ya kupigia chepuo usawa wa wanawake. Maandamano  hayo yatafanyika pia sehemu mbali mbali duniani.