Ofisi ya Haki za binadamu yasikitishwa na hukumu ya kifo Indonesia

Ofisi ya Haki za binadamu yasikitishwa na hukumu ya kifo Indonesia

Ofisi ya haki za binadamu imeisihi serikali ya Indonesia kujizuia kuwakatia hukumu ya kifo watu wamepatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.

Msemaji wa Ofisi hiyo Rupert Colville, amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva akisema wanasikitishwa na taarifa ya kunyongwa kwa washtakiwa sita mwezi Januari.

Kwa mujibu wa Colville, watu wengine kadhaa wanatarijiwa kunyongwa hivi karibuni na ameiomba serikali ya Indonesia iwasamehe.

“ Jitihada zisizoisha za Indonesia kupambana na janga la biashara ya madawa ya kulevya zinasikika, lakini njia hii si sahihi. Kwa kuchukua msimamo huo, Indonesia itashindwa sasa kupigania haki za raia wa Indonesia ambao wamekatiwa adhabu ya kifo kwenye nchi zingine. “

Msemaji huyo ameongeza kwamba, katika nchi ambazo hazijaondoa adhabu ya kifo, ofisi ya haki za binadamu inashauri kutumia hukumu ya kifo kwa uhalifu wa kuua kwa kukusudia.

Halikadhalika amesema hakuna thibitisho kwamba adhabu ya kifo inawazuia watu wengine kujiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya.