Ban asikitishwa na kutokamilishwa kwa mazungumzo kuhusu Sudan Kusini
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea masikitiko yake kutokana na kutohitimishwa kwa mafanikio mchakato wa amani wa Sudan Kusini unaoratibiwa na jumuiya ya IGAD.
Halikadhalika Ban amesitikishwa na kitendo cha Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na na makamu wake wa zamani Riek Machar kushindwa kuonyesha uongozi wao na kufikia makubaliano juu ya serikali ya pamoja.
Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema kwa zaidi ya siku mbili Bwana Ban amekuwa akiwasiliana na pande hizo kinzani Sudan Kusini pamoja na viongozi wa ukanda huo akitoa wito wa kuendelea kwa mashauriano.
Hata hivyo licha ya hatua hiyo ya kutia masikitiko, Katibu Mkuu amesihi kwa dhati pande hizo zijizuie kutofanya jaribio lolote linaloweza kuchochea zaidi mzozo huo huku akisema nguvu za kijeshi si mbadala wa mashauriano.
Amesifu jitihada za IGAD na mjumbe maalum wa chombo hich huko Sudan Kusini za kutaka kuleta amani na ameunga mkono azma ya IGAD ya kutaka kupanua wigo wa wadau kwenye mchakato huo wa amani.
Ban amerejelea azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama namba 2206 la mwaka huu wa 2015 linaloonyesha nia ya chombo hicho kuweka vikwazo lengwa kwa watu na vyombo maalum iwapo watashindwa kuzingatia makubaliano ya kusitisha chuki yaliyotiwa saini mwezi Januari mwaka jana.