Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusikubali uharibifu huu wa ISIL kwenye mali za kale: UNESCO

Tusikubali uharibifu huu wa ISIL kwenye mali za kale: UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO limelaani vikali uharibifu uliofanywa kwenye maeneo ya kumbukumbu ya vitu vya kale huko Nimrud nchini Iraq.

Uharibifu huo umefanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la ISIL ambapo Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema uharibifu huo unakumbusha jamii ya kimataifa kuwa hakuna kilicho salama nchini Iraq.

Amesema ISIL siyo tu wanalenga uhai wa binadamu na makundi ya pembezoni pekee bali pia wanalenga kutokomeza kabisa historia na urithi wa binadamu.

Hata hivyo amesema haipaswi kunyamaza kwani uharibifu huo wa makusudi ni uhalifu na ametoa wito kwa viongozi wa kidini na kisiasa kwenye eneo hilo kusimama kidete na kukumbusha kuwa hakuna sababu yoyote iwe ya kisiasa au kidini inayohalalisha kitendo hicho.

Bi. Bokova ametoa wito kwa yeyote anayeweza hususan vijana nchini Iran na kwingineko kuchukua hatua kulinda urithi huo kwani ni mali yao huku akisihi wasomi na taasisi za makumbusho kuelezea umuhimu wa mali hizo na ustaarabu wa Mesopotamia.

Mji wa Nimrud ambao mali zake za kale zimeharibiwa ulianzishwa zaidi ya miaka 3,300 na ulikuwa ni moja ya miji mikuu ya dola la Assyria