Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kuliwekea uzito swala la ujangili

Ni wakati wa kuliwekea uzito swala la ujangili

Mwaka 2013, tembo 20,000 wameuawa kutokana na ujangili, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa akiongeza kwamba ujangili, licha ya kuathiri mazingira na bayoanuai, unahatarisha hali ya usalama.

Bwana Kutesa amesema hayo wakati akihutubia mkutano maalum wa baraza hilo uliofanyika leo katika kuadhimisha siku ya mazao ya porini.

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema ingawa jitihada zimefanyika kudhibiti uwindaji haramu, kama mfano makubaliano kuhusu biashara ya kimataifa ya viumeb vilivyo hatarini kutoweka, (CITES), bado ushirikiano wa kimataifa unapaswa kuimarishwa ili kusitisha uuzaji na ununuaji haramu wa wanyamapori.

Ametaja mfano wa udhibiti mpakani, au uelimishaji wa jamii zinazoishi na wanyama hao.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson, amesema sababu za kuongezeka kwa ujangili ni ukosefu wa utawala bora na ufisadi.

Aidha amesema uzalishaji wa bidhaa unaotumia viumbe vya wanyamapori unapaswa kusitishwa iwapo dunia inataka kutokomeza ujangili.

Bwana Eliasson pia amesisitiza athari za ujangili kwa amani na usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu, amesema bado juhudi za mashirika ya kimataifa zinahitajika .

“ Kwenye siku hii ya wanyamapori duniani, tutumie ujumbe mzito kwa watumiaji wote, wauzaji na serikali zote kwamba tumeungana dhidi ya ujangili na watekelezaji wake. Ujangili ni hatari kwa mustakhabali endelevu. Ni dharau na ukosefu wa heshima kwa maisha yaliyopo ulimwenguni, yawe yale ya binadamu, wanyama au majani.”