Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kibinadamu yahaha kuwanusuru wakimbizi wa Samarra

Mashirika ya kibinadamu yahaha kuwanusuru wakimbizi wa Samarra

Wadau wa misaada ya kibinadamu wanawasilisha huduma muhimu kwa maelfu ya familia katika wilaya ya Samarra nchini Iraq kufuatia mashambulizi katika jimbo la Salah al-Din.

Misaada hiyo inajumuisha ile iliyopelekwa na misafara mitatu ya magari ikiwa imesheheni maji na huduma za kujisafi iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto UNICEF kwa watu 24,000.

Kwa upande wake Shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR limetuma shehena ya bidhaa za vyakula kutoka Baghdad kwa familia 500.

Nalo Shirika la mpango wa Chakula Duniani(WFP) litatuma msaada wa chakula wa dharura kesho Alhamisi na katika wiki chache zijazo huku Shirika la Afya Duniani(WHO) likitoa huduma za afya kulingana na mahitaji na litatoa chanjo dhidi ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, mashirika yasiyo ya kiserikali yanasaidia kuandikisha familia za watu waliofurushwa makwao na mifuko ya chakula na bidhaa zisizo chakula

Mratibu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Lise Grande amesema kwamba wanasikitishwa na hali ya kibinadamu Samarra akiongeza kuwa wanafahamu kwamba watu wanamahitaji mengi na hivyo wanafanya kila liwezekanalo kuwasaidia.

Mapigano ya wiki chache zilizopita kati ya vikosi vya usalama vya Iraq (ISF) na kikundi cha kigaidi cha ISIL huko Salah al-Din yamesababisha maelfu ya watu kukimbia kutoka wilaya ya Daur na kwingineko kwenye eneo hilo.