Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani mauaji ya mwanahabari nchini Colombia

UNESCO yalaani mauaji ya mwanahabari nchini Colombia

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamduni UNESCO Irina Bokova amelaani mauaji ya mwandishi wa habari Luis Carlos Peralta Cuéllar ambaye aliuwawa mnamo Februari 14 karibu na nyumbani kwake nchini Colombia.

Taarifa ya UNESCO imemkariri Bi. Bokova akizitaka mamlaka nchini humo kuwafikisha katika vyombo vya sheria watekelezaji wa mauaji hayo huku akisisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari ambao amesema ni nguzo ya demokraisa na utawala bora. Ametaka wanahabari kuachwa kutekeleza majukumu yao bila kuhofia maisha yao.

Mwanahabari Luis Carlos Peralta Cuéllar mwenye umri wa miaka 63 alikuwa mmiliki na Mkurugenzi wa kituo cha redio kiitwacho Linda na wakati wa utendaji wake alikuwa akiandika mara nyingi kuhusu kashfa za rushwa na hivyo alipokea vitisho mara kadhaa.