Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama latangaza vikwazo kwa wanaovuruga amani Sudan Kusini

Baraza la Usalama latangaza vikwazo kwa wanaovuruga amani Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja limeptisha azimio la kuweka vikwazo vya usafiri kwa watu ambao Kamati ya Vikwazo ya Baraza hilo itawataja kuwa  wameshiriki moja kwa moja au kwa njia nyingine katika vitendo vinavyohatarisha amani, usalama na ustawi wa taifa la Sudan Kusini. Pamoja na vikwazo vya usafiri kwenda nchi za nje, mali za watu hao pia zitafungiwa.

Kwa mantiki hiyo, Baraza la Usalama limeitaka Kamati ya Vikwazo iwatambue watu ambao wanapaswa kulengwa na vikwazo hivyo.

Kwa mujibu wa azimio hilo namba 2206 (2015), vikwazo hivyo vitajumuisha vitendo ambavyo vinasababisha kuendeleza mgogoro wa Sudan Kusini au kuvuruga mazungumzo ya amani na maridhiano, vikiwemo kukiuka vipengele vya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Vikwazo hivyo pia vitawalenga wanaotenda vitendo au kuandama sera zinatishia mchakato wa amani Sudan Kusini, pamoja na wanaopanga na kuongoza utekelezaji wa vitendo vinavyokiuka sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na sheria ya kibinadamu, au vitendo vinavyolingana na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini.

Azimio linawalenga pia watu ambao wanawalenga raia, wakiwemo wanawake na watoto, kupitia vitendo vya ukatili, vikiwemo mauaji, ulemazaji, utesaji, ubakaji au ukatili wa ngono, utekaji nyara, ushambuliaji wa shule, hospitali, majengo ya ibada au sehemu wanakotafuta makazi raia waliokimbia machafuko.

Vikwazo hivyo pia vitawalenga wanaosajili au kutumia watoto katika jeshi au makundi yenye silaha, uvurugaji wa shughuli za ulinzi wa amani na diplomasia, na mashambulizi dhidi ya ujumbe wa Umoja wa Maatifa, walinda amani wa kimataifa na wahudumu wa kibinadamu.

Akizungumza baada ya kupitishwa azimio hilo, mwakilishi wa kudumu wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa, Francis Deng, amesema vikwazo havitaleta suluhu endelevu kwa mzozo uliopo nchini mwake

(Sauti ya Deng)

Viongozi wa Sudan Kusini wamesema mara kwa mara kuwa vikwazo vinatishia kuvuruga mchakato wa amani. Swali muhimu ni, je, vikwazo ni adhabu kwa kushindwa kuafikia amani au kichochezi cha kuafikia amani? Iwapi ni adhabu, basi linaishia hapo. Lakini iwapo ni kichochezi cha kuafikia amani, basi vinakuwa ni vyenye kuibua shinikizo lisilo zuri, ambalo linaweza tu kuibua hatua zinazoweza kuvuruga hali zaidi.”