Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama kuzuru Afrika mwezi huu:

Baraza la usalama kuzuru Afrika mwezi huu:

Wakati Ufaransa inachukua urais wa baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Machi, Mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, François Delattre, amewaambia waandishi wa habari leo mjini New York kwamba Afrika itakuwa kipaumbele cha kwanza katika kipindi cha urais wake.

Amesema wajumbe wa Baraza la Usalama watakuwa ziarani barani Afrika kuanzia Machi 9 hadi tarehe 13, wakitembelea Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ethiopia na Burundi.

“ Lengo letu kuu la ziara hii ni kusisitiza jinsi tunajali nyakati za mpito wa kisiasa na ulinzi wa amani kwenye bara la Afrika.

Kipaumbele cha pili ni kupitisha azimio la kuongeza muda wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Ufaransa amewakumbusha waandishi wa habari kwamba ni azimio muhimu kwani MONUSCO, ambayo jukumu lake ni kutunza raia, ni operesheni kubwa zaidi katika historia ya Umoja wa Mataifa, na mzozo wa DRC umeshasababisha vifo vipatavyo milioni 5

Lengo la azimio jipya ni kuimarisha MONUSCO lakini vile vile kupunguza idadi ya walinda amani.

Aidha kipaumbele cha tatu ni swala la watoto wanaotumikishwa vitani, ambalo litajadiliwa katika baraza la usalama mwezi huu.

Halikadhalika Bwana Delattre ametaja mizozo ambayo itaangaziwa wakati wa urais wake kuwa ni Libya, Yemen na Ukraine halikadhalika suala la Boko Haram kwa lengo la kuhusisha zaidi Muungano wa Afrika.