Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Nigeria wazidi kumiminika Cameroon

Wakimbizi wa Nigeria wazidi kumiminika Cameroon

Takribani raia 16,000 wa Nigeria, wamekimbilia kaskazini mwa Cameroon mwishoni mwa wiki iliyopita kufuatia mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR linashirikiana na serikali ya Cameroon ili kuwahamishia wakimbizi hao mbali na maeneo ya mapigano na kuwapatia chakula pamoja na huduma za maji na afya.

Hata hivyo UNHCR imeongeza kwamba haiwezi kufikia maeneo ya mpakani kwa sababu mapigano yanaendelea pia kwa upande wa Cameroon.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

“ Misafara ya uhamisho kutoka mpakani hadi Kousseri itaanza kesho ikihamishia wakimbizi 2,000 kila siku. Kwa sababu ya kuzorota kwa hali ya usalama kwenye eneo hilo, tunajadiliana kuhusu kufungua kambi ya pili ya wakimbizi mbali zaidi ya maeneo ya mpakani yasiyokuwa na usalama”

UNHCR inakadiria kwamba idadi ya wakimbizi nchini Caemroon ni takriban 66,000, wengine 18,000 wakiwa wametafuta hifadhi nchini Chad, na wengine milioni Moja wakiwa ni wakimbizi wa ndani kaskazini wa Nigeria.