Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuimarishe usaizidi endelevu kwa nchi zilizokumbwa na Ebola: Clark

Tuimarishe usaizidi endelevu kwa nchi zilizokumbwa na Ebola: Clark

Umoja wa Mataifa umetoa rai kwa jamii ya kimataifa kuimarisha usaidizi endelevu kwa mataifa matatu ya Afrika Magharibi ambayo yameathirika zaidi na mlipuko wa Ebola. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grece)

Mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja huo, UNDP Hellen Clark amesema hayo huko Brussels Ubelgiji wakati akifungua mkutano wa kimataifa kuhusu hali ya Ebola akisema usaidizi huo unahitajika ili kutokomeza vikwazo vya maendeleo vilivyotokana na mlipuko huo.

Mathalani amesema ni lazima kuhakikisha jitihada za kuzikwamua nchi hizo ambazo ni Liberia, Sierra Leone na Guinea zinashughulikia vichochezi vilivyosababisha kuibuka na kusambaa haraka kwa Ebola.

Bi. Clark ambaye hivi karibuni alitembea nchi hizo ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kujenga mifumo thabiti ya huduma na kupatia kipaumbele maendeleo ya wananchi na uwezeshaji wa raia.

Vipaumbele vingine ni kukidhi mahitaji ya manusura wa Ebola, yatima na vikundi vingine ambavyo vimeathirika na mlipuko wa Ebola bila kusahau kuimarisha mifumo ya afya na kujenga fursa za kujikwamua kiuchumi hasa kwa kaya ambazo zinaendeshwa na wanawake pekee.