Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaag afanya mazungumzo na viongozi wa muungano wa Kiarabu kuhusu Lebanon

Kaag afanya mazungumzo na viongozi wa muungano wa Kiarabu kuhusu Lebanon

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon Sigrid Kaag amekutana na Katibu Mkuu wa muungano wa falme za kiarabu Nabil el Araby na viongozi waandamizi wa serikali ya Misri mjini Cairo hapo jana ambapo viongozi hao wamejadili hali nchini Lebanon na maendeleo katika ukanda huo.

Kadhalika viongozi hao wamejadili utekelezaji wa azimio la baraza la usalama nambari 1701 la mwaka 2006.

Bi Kaag na washiriki wa mazungumzo hayo wamejadili umuhimu wa usalama endelevu, na uhitaji wa utulivu wa Lebanon katika mazingira magumu ya ukanda huo. Wamesema utulivu katika nchi hiyo unajumuisha suluhu la ombwe la nafasi ya uongozi huku mratibu huyo maalum wa Umoja wa Mataifa akisema katika siku 83 Lebanon itakuwa na mwaka mmoja bila Rais .

Amesisitiza umuhimu wa mkutano wa kimataifa wa ahadi za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Syria na Kuwait ni fursa kwa Lebanon na washirika wake wa kimataifa katika kupata misaada endelevu ya kimataifa kwa ajili ya nchi hiyo.