Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza lalaani ukatili unaofanywa na ISIL huko Iraq

Baraza lalaani ukatili unaofanywa na ISIL huko Iraq

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameshutumu vikali mwendelezo wa vitendo vya kikatili vinavyofanywa na kikundi cha kigaidi cha ISIL au Da’esh nchini Iraq na Syria.

Katika taarifa yao, wajumbe hao wametaja vitendo hivyo kuwa ni pamoja na kuteka nyara watu wa jamii ya Sunni kutoka Tikrit siku ya Jumatano na uharibifu wa makusudi wa mali za kidini na kitamaduni kwenye jumba la makumbusho mjini Mosul.

Wameeleza wasiwasi wao kuwa ISIL na vikundi vingine vyenye uhusiano na kikundi cha kigaidi cha Al Qaeda wanajipatia kipato kwa kuuza mali hizo za urithi wa kitamaduni wanazopora wakisema kundi hilo la ISIL ni lazima lishindwe katika vita vinavyoendelea.

Wamehadharisha kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa na ISIL si kitisho chochote kwa baraza la usalama na badala yake vinaimarisha azma ya baraza hilo ya kutaka ushirikiano baina a serikali na taasisi kwenye ukanda huo ili kutokomeza kundi hilo.

Wajumbe wamesema hakuna kitendo chochote cha ghasia kinachoweza kubadili mwelekeo wa kusaka amani, demokrasia na ujenzi wa Iraq.

Hata hivyo wamekumbusha mataifa kuwa harakati zozote za kukabiliana na ugaidi ni lazima zizingatie sheria za kimataifa hususan haki za kimataifa za binadamu, ukimbizi na usaidizi wa kibinadamu.