Watu bilioni 1.1 wamo hatarini kupoteza uwezo wa kusikia- WHO

27 Februari 2015

Barubaru na vijana wapatao bilioni 1.1 wamo hatarini kupoteza uwezo wa kusikia kwa sababu ya matumizi yasiyo salama ya vidude kama simu za kisasa na kuwa katika mazingira ya burudani yenye kiwango cha juu cha kelele kama vile disko, vilabu vya pombe na mashindano ya michezo, limeonya Shirika la Afya Duniani, WHO.

Kwa mujibu wa WHO, kupoteza uwezo wa kusikia kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya mwili na akili, elimu na ajira.

Takwimu zilizotathminiwa na WHO kutoka utafiti uliofanywa katika nchi zenye vipato vya wastani na vya juu, zinaonyesha kuwa miongoni mwa barubaru na vijana kati ya umri wa miaka 12 na 35, asilimia 50 kati yao hujitia kwenye hatari ya madhara yatokanayo na kelele za sauti za vidude vya kucheza muziki, huku asilimia 40 wakijikuta kwenye maeneo ya burudani yenye kelele zinazoweza kudhuru masikio.

Kwa mujibu wa WHO, viwango vya sauti visivyo salama ni vile vinavyozidi desibeli (dB) 85 kwa kipindi cha saa 8 au dB100 kwa muda wa dakika 15.

Mkurugenzi wa WHO wa idara ya udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ulemavu, ukatili na uzuiaji wa mejeraha, Dkt. Etienne Krug, amesema kuwa vijana wengi wanapofurahia maisha yao kila siku, wanajiweka katika hatari ya kupata ulemavu wa kusikia, akionya kuwa wanapaswa kujua kuwa ukishapoteza uwezo wako wa kusikia, hautarejea.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter