Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 377 zahitajika kwa usaidizi wa kibinadamu Mali- OCHA

Dola milioni 377 zahitajika kwa usaidizi wa kibinadamu Mali- OCHA

Mashirika ya kibinadamu nchini Mali yanahitaji dola milioni 377 ili kukidhi mahitaji ya watu wanaozidi milioni 1.5 mwaka wa 2015, imesema Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura, OCHA. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kufadhili awamu ya pili ya mpango wa pamoja wa mashirika hayo kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2016.

Kwa mujibu wa OCHA, licha ya hatua zilizopigwa katika kukarabati na kurejesha ustawi katika maeneo yaliyoathiriwa kaskazini mwa Mali, kutokuwepo usalama kunaathiri kurejeshwa kwa huduma muhimu za msingi na kuanza tena shughuli za kiuchumi.

Kwa sababu hiyo, mamia ya maelfu ya watu nchini Mali bado wanahitaji msaada wa kibinadamu ili kuishi. Jens Laerke ni msemaji wa OCHA.

(Sauti ya Jens Larke)

“Kwa kweli, tunakadiria kwamba idadi kubwa ya watu wataathirika na ukosefu wa usalama wa chakula mwaka huu, na kwa kuwa karibu nusu ya raia wa Mali ni watoto, takriban watoto 715,000 wataathirika na utapiamlo wa kupindikia”

Mpango wa miaka mitatu ya usaidizi wa kibinadamu Mali, ambao unajumuisha mashirika 40 ya kibinadamu yakiwemu ya Umoja wa Mataifa, ulizinduliwa na mnamo mwaka 2014, ukilenga kukidhi mahitaji ya hivi sasa ya watu walio hatarini zaidi, huku ukijikita katika kuboresha maisha na uthabiti wa jamii zilizoathirika.