Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tufanye kila liwezekanalo kumkomboa mwanamke :Ban

Lazima tufanye kila liwezekanalo kumkomboa mwanamke :Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amesema ni lazima kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha mwanamke anakombolewa katika nyanja zote , kuanzia kwenye Umoja wa Mataifa , katika serikali kote duniani  na katika nyanja ya biashara. Taarifa ya Flora Nducha inaeleza zaidi..

(Taarifa ya Flora)

Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu wanawake katika uongozi na ngazi ya maamuzi huko Santiago Chile , Ban amesema japo hatua inakwenda taratibu lakini nchini nyingi duniani zimeanza kutoa haki kwa wanawake, sasa wanaweza kupiga kura, wanaongoza sekta za biashara na wanashika nafasi za juu serikalini.

Ameongeza kuwa Umoja wa mataifa umepiga hatua kubwa tangu mwaka 1979 baraza kuu lilipitisha mkataba wa kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake CEDAW, 1995  ulipoandaa mkutano wa Beijing hadi 2000 baraza la usalama lilipopitisha azimio la kihistoria kuhusu wanawake, amani na usalama.

Akimshukuru Rais wa Chile Michele Bachelet  kuwa mwenyeji wa mkutano huo Ban amesema anajivunia kuteuwa wanawake wengi kwenye ngazi za juu Umoja wa Mataifa

(SAUTI BAN)

Ninajivuna kwa kuteuwa wanawake wengi kwenye ngazi za maamuzi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Umoja wa Mataifa. Wanawake wanainuka juu kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa na katika ofisi zetu duniani kote”

Ameongeza kuwa mkutano maalumu wa maendeleo endelevu utakaofanyika Septemba hapa New York utakuwa na agenda muhimu itakayothamini jukumu la wanawake. Na jitihada ziko dhahiri kwani hadi sasa dunia ina wanawake 20 ambao ni viongozi wa taifa.