Mabadiliko ya tabianchi si ongezeko la joto tu: WMO

27 Februari 2015

Mabadiliko kwenye mfumo wa mvua na ukosefu wa usalama wa chakula ni miongoni mwa matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na ongezeko la halijoto.

Kwa mujibu wa Michel Jarraud, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Hali ya hewa duniani, WMO, sekta zote za uchumi na raia wenyewe wanaweza kuathirika na mabadiliko ya tabianchi, ambayo matokeo yake yote hayajulikani vizuri.

Jarraud ameeleza kwamba WMO imeyaweka kipaumbele maswala manne katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi nayo ni swala la majanga, matatizo ya afya, usalama wa chakula na upatikanaji wa maji.

Amesema wakati watu wengi wanajua kwamba mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ongezeko la halijoto, wachache wanatambua athari katika mfumo wa mvua.

« Tayari tunaona kwamba baadhi ya sehemu zinakosa mvua. Tunaona kwamba ukame unarudia mara kwa mara na unazidi kuwa mkali. Kwenye sehemu zingine, tunaona kwamba mafuriko hurudia mara kwa mara, na ni makali zaidi.. Kwa hiyo tunaona vurugu katika mfumo wa mvua, na hii ni sekta muhimu ya kuiweka kipaumbele »

Amekariri kwamba, ikiwa hatua hazitachukuliwa haraka, nchi nyingi hususani zinazoendelea zitshindwa kumudu gharama za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi .

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud