Heko Paraguay kwa matumizi ya nishati endelevu:Ban

26 Februari 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani huko Amerika ya Kusini amehutubia bunge la Paraguay akigusia masuala ya ugaidi, mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa amani na umuhimu wa kuwapatia fursa wanawake.

Mathalani kuhusu ugaidi amesema hakuna nchi au taasisi inayoweza kudhibiti kero hiyo peke yake, bali nchi, taasisi za kikanda na kimataifa na makundi yote kwenye jamii yanapaswa kushikamana na kuibuka na mkakati mtambuka unaoweza kujenga mustakhbali wa kuheshimu sheria za haki za binadamu na kimataifa.

Amesema kwa mantiki hiyo miezi michache ijayo ataitishisha mkutano wa viongozi wa kidini duniani utakaofanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa ili kuweka msisitizo wa umuhimu wa mshikamano, kustahimiliana na maelewano.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Ban ambaye ametembelea bwawa la ITAIPU nchini Paraguay linalolozalisha umeme kwa nguvu za maji, amesema huo ni mfano wa jinsi nchi hiyo ilivyo bingwa wa nishati endelevu kwani umeme wote unatokana na nguvu za maji.

Akizungumzia uwezeshaji wanawake, Ban amesema  nchini Paraguay kama ilivyo nchi zingine, sheria za kuwawezesha wanawake zipo lakini tatizo ni utekelezaji kama ilivyo nchi zingine.

Amesema ni lazima pengo hilo liondolewe kwa kuwa hakuna taifa au jamii inayoweza kusonga mbele iwapo nusu ya watu wake wanakandamizwa.

Kutoka Paraguay, Katibu Mkuu anaelekea Chile ambako atashiriki mkutano wa kimataifa kuhusu wanawake na uongozi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud