Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa UNISFA Abyei

Baraza la Usalama laongeza muda wa UNISFA Abyei

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja wameptisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Usalama kwa eneo la Abyei hadi tarehe 15 Julai, 2015.

Baraza hilo pia limekaribisha mikakati ya UNISFA ya kusaidia katika kuanza tena mashauriano ya kijamii na katika utawala wa kijamii chini ya kamati ya pamoja ya uangalizi na usimamizi wa Abyei, AJOC.

Katika azimio hilo, wajumbe wa Baraza la Usalama pia wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kwa ushirkiano kati ya serikali za Sudan na Sudan Kusini, ambao wamesema ni muhimu kwa ajili ya kudumisha amani, usalama, na ustawi, na uhusiano kati ya nchi hizo mbili siku zijazo.

Baraza la Usalama pia limeamua kuwa idadi ya askari walioidhinishwa chini ya azimio namba 2104(2013) idumishwe, na kwamba vikosi vilivyosalia viendelee kupelekwa Abyei.

Wajumbe wa Baraza la Usalama pia wamelaani uwepo wa vikosi vya polisi vya Diffra kwenye eneo la Abyei, na kutaka serikali ya Sudan iviondoe vikosi hivyo, likikariri matakwa ya maazimio yake ya awali kuwa eneo la Abyei halipaswi kuwa na vikosi vyovyote au watu wenye silaha ila vikosi vya UNISFA na polisi wa kutoa huduma za umma Abyei.

Akizungumza baada ya kupitishwa azimio hilo, mwakilishi wa kudumu wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa, Dafalla Al-Haj Ali, amesema..

(Sauti ya Ali)

“Azimio hili ambalo limepitishwa limepitishwa, katika aya zake nyingi limesisitiza umuhimu wa kutekeleza makubalianoyaliyosainiwa kati ya Sudan na Sudan Kusini kwa ajili ya Abyei. Azimio hili limesisitiza kuwa kupatia suluhu hali hii kunawezekana tu kupitia mazungumzo kati ya pande hizo mbili. Kwa hiyo tunatoa shukrani zetu kwa kupitishwa azimio hili.”

Naye mwakilishi wa kudumu wa Sudan Kusini Francis Deng akasema..

(Sauti ya Deng)

“Tunakaribisha ripoti ya Katibu Mkuu na kuongeza kwa mamlaka ya UNISFA kwa azimio hili ambalo mmeptisha. Katika ripoti ya Katibu na azimio hili, masuala muhimu yanayohusu usalama na hatma ya watu wa Abyei kwa ujumla. Kama nilivyosema mara nyingi, kupelekwa kwa vikosi vya UNISFA ndilo huenda ndilo jambo muhimu zaidi lililowahi kutokea kwa watu wa eneo hilo katika miongo mingi.”