Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na machafuko Venezuela

Ban asikitishwa na machafuko Venezuela

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki- Moon amesikitishwa na taarifa za machafuko na kupotea kwa maisha ya watu nchini Venezuela huku akielezea na kufurahishwa na tamko la serikali kufanya uchunguzi wa kina .

Katibu Mkuu pia amepongeza hatua ya mazungumzo kwa njia ya simu kati yake na Katibu Mkuu wa Shirika la Mataifa ya Marekani (OAS) mnamo Februari 20, yaliyojikita katika ujenzi wa demokrasia kwa ajili ya majadiliano nchini Venezuela.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imesema pia Bwana Ban ameunga mkono juhudi za hivi karibuni kutoka kwa Katibu Mkuu wa umoja wa mataifa ya Marekani Kusini (UNASUR) kuanzisha tena mazungumzo kati ya serikali na wawakilishi wa upinzani yaliyoanza Aprili mwaka jana yakiungwa mkono na UNASUR na uongozi wa Holy See ambayo ni mamlaka inayowakilisha Vatican kwenye Umoja wa Mataifa.

UNASUR na Holy See wanasaidia Venezuela katika kukabiliana na changamoto zinazoikumba nchi hiyo na kuhakikisha haki za binaadamu kwa raia wa nchi.

Ban amekaribisha tangazo la Katibu Mkuu wa UNASUR la ziara ya siku za usoni nchini Venezuela kwa uwakilishi maalum kupitia waziri wa mambo ya nje.