Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo la uchunguzi lashukuru ushirikiano kutoka Mali

Jopo la uchunguzi lashukuru ushirikiano kutoka Mali

Jopo lililokuwa linachunguza ghasia zilizoibuka kwenye mji wa Gao nchini Mali tarehe 27 mwezi uliopita limehitimisha ziara yake ya siku nane nchini humo iliyowakutanisha na makundi mbali mbali ikiwemo viongozi wa serikali.

Kwa mujibu wa taarifa, jopo hilo la ngazi ya juu lililoteuliewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa lilikuwa na mazungumzo pia na viongozi wa mji wa Gao, polisi, wawakilishi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, viongozi wa kijamii, waandamanaji waliojeruhiwa wakati wa tukio hilo, familia za wahanga, halikadhalika watu waliosaidia kuangazia tukio hilo.

Kwa sasa jopo hilo la wataalamu huru watatu wenye uzoefu wa kimataifa linaelekea New York, Marekani ili kuwasilisha ripoti  ya awali kwa Katibu Mkuu huku ripoti kamili ikitarajiwa mwishoni mwa mwezi ujao.

Wataalamu hao ni Bacre Waly Ndiaye kutoka Senegal, Mark Kroeker  wa Marekani na Ralph Zacklin wa Uingereza na wameshukuru kwa ukarimu na ushirikiano waliopatiwa wakati wakitekeleza jukumu lao nchini Mali.