Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yazindua mpango wa kusaidia elimu ya vijana Syria

UNESCO yazindua mpango wa kusaidia elimu ya vijana Syria

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limezindua mpango wa kupunguza mianya ya elimu kwa vijana ambao wameathiriwa na mzozo nchini Syria.

Mzozo wa Syria unaingia mwaka wa tano, na umechangia matatizo makubwa ya kibinadamu na maendeleo, na hivyo kuvuruga upatikanaji wa elimu bora katika nchi zilizoathiriwa.

Tangu mzozo huo ulipoanza, zaidi ya watoto milioni 3 na vijana wamelazimika kuacha shule nchini Syria. Tathmini ya hivi karibuni imeonyesha kuwa kuna mwanya wa hadi asilimia 70 katika kusoma kwa kizazi cha vijana wa Syria wakimbizi, kati ya umri wa miaka 15 na miaka 30 , ambao hawapati elimu bora na nafasi za mafunzo muhimu.

Mpango huo wa UNESCO wa miaka miwili uitwao ‘kuziba mianya ya elimu kwa vijana’, utasaidia kuwezesha upatikanaji wa elimu bora ya sekondari na taasisi za kitaaluma pamoja na kuimarisha mifumo ya elimu ya nchi zilizoathiriwa, hususan Syria, Jordan, Lebanon na Iraq.