Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utambuaji wa waathirika ni muhimu katika vita dhidi ya utumwa Ubelgiji

Utambuaji wa waathirika ni muhimu katika vita dhidi ya utumwa Ubelgiji

Mtaalamu maalumu wa Umoja wa mataifa Urmila Bhoola leo ametoa wito kwa serikali ya Ubelgiji kuimarisha vita vyake dhidi ya mifumo yote ya utumwa kwa kujikita zaidi katika ugunduaji sahihi na kuwatambua waathirika.

Amesema anakaribisha uwepo wa kitengo maalumu cha uchunguzi wa madai ya unyonyaji wa mazingira ya kitumwa ndani ya mifumo ya kijamii, kazi na polisi nchini Ubelgiji. Mtaalamu huyo ameyasema haya wakati akihitimisha ziara yake ya siku nane nchini humo.

Amesema hata hivyo waathirika walio hatarini kama watoto na makundi mengine hawagunduliki kila wakati na kufikishwa katika vyombo maalum vya kuwasaidia na hivyo wanaachwa katika hatari ya kunyonywa na kunyanyaswa.

Bi Bhoola amesistiza haja ya kuhakikisha kwamba wahusika wote walio msitari wa mbele wakiwemo polisi , huduma za afya na jamii pamoja na walezi wa watoto wasiokuwa na wazazi wanapatiwa mafunzo muhimu ya kuwatambua waathirika wa mifumo yote ya kisasa ya utumwa.

Mwakilishi huyo atawasilisha ripoti ya utafiti wake na mapendekezo kwenye kikao maalumu cha baraza la haki za binadamu mwezi Septemba mwaka huu.