Ukosefu wa utaifa unawaathiri zaidi ya watu milioni 10 duniani

25 Februari 2015

Serikali zinapaswa kuchukua hatua ili kubadilisha sheria ya utaifa ili kutatua shida ya watu waliokosa utaifa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR.

Makadirio ya UNHCR ni kwamba watu hao ni milioni 10 duniani, zaidi ya 700,000 wakiwa kwenye ukanda wa Afrika ya Magharibi, ambao hatma yao inazungumziwa mjini Abidjan kwenye mkutano wa mawaziri kuhusu ukomeshwaji wa kutokuwa na utaifa.

Emmanuelle Mitte ni mtalaam wa maswala ya ukosefu wa utaifa kwenye UNHCR.

“ utaifa unakupa haki ya kuwa na haki. Mtu ambaye hana utaifa hatambuliwi na nchi yoyote, ni mtu ambaye anateseka, kwa sababu haki zake za msingi zinakataliwa”

Katika mkutano huo Kamishna Mkuu wa UNHCR, Antonio Guterres amezipongeza nchi zilizopo Afrika ya Magharibi ambazo zimeanza kubadilisha sheria za utaifa ili kutokomeza tatizo hilo. Amesema lengo la UNHCR ni kulitokomeza kabisa tatizo hilo katika kipindi cha miaka 10.

Emmanuelle Mitte ameiambia redio ya Umoja wa Mataifa kwamba mabadiliko ya sheria ya utaifa yanaweza kutekelezwa kwa uraisi.

“ Hatua ya kwanza ni kuhesabu idadi ya watu waliokosa utaifa, na kuelewa ni watu gani na kwa nini wamekosa utaifa. Serikali zikishaelewa sababu ya ukosefu wao wa utaifa, zitaweza kuchukua hatua ili kuzuia visa vipya vya ukosefu wa utaifa. Kwa mfano kuwapatia utaifa watoto wote wanaozaliwa nchini humo. Wakifanya hivo, basi watachangia sana katika kupunguza ukosefu wa utaifa. Na kubadili sheria hakuhitaji pesa nyingi”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud